LINDENI MFUKO KWA KUREJESHA MKOPO UWAFIKIE WENGI

  • 25 October, 2023
LINDENI MFUKO KWA KUREJESHA MKOPO UWAFIKIE WENGI

Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bwana Gerson Msigwa leo tarehe 13 Oktoba, 2023 ametoa rai kwa wasanii kuwa mstari wa mbele kuulinda Mfuko wa Utamaduni kwa kufanya marejesho kwa wakati ili uweze kuendelea kutoa kwa wengine na kuinua Sekta ya sanaa nchini.

Ameyasema hayo wakati alipotembelea Ofisi za Mfuko wa Utamaduni na Sanaa kisha kuongea na baadhi ya wasanii ambao tayari wameshanufaika na mikopo hiyo inayotolewa na Serikali kwa lengo la kuwainua wasanii nchini.

"Hizi fedha zinategemea mzunguko wake kwahiyo unapochukua mkopo huo hakikisha unarejesha kwa wakati ili wengine wapate na kuufanya hai wakati wote" amesema Msigwa.

Ameendelea kusema kuwa, Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuinua sekta ya sanaa kwakuwa ina umuhimu mkubwa sana kwa jamii hasa ikibadilishwa na kuwa bidhaa inayoweza kurejesha utimamu wa mwili na akili kupitia burudani.

Ameongeza kuwa, Sekta ya Sanaa inaendana na mabadiliko ya teknolojia hivyo wasanii lazima wataendelea kuhitaji huduma ya mikopo kwahiyo ni wajibu kuhakikisha wanaendelea kuthamini juhudi za Serikali kwa kuutunza Mfuko wa Utamaduni wakati wote.

Kwa upande wao wasanii walionufaika akiwemo Muhsin Awadhi (Dkt. Cheni) na Abdul Msanga kwa nyakati tofauti wameishukuru Serikali kwa kuwapa thamani kuanzisha mfuko huo unaoshirikiana na Benki ambapo umewawezesha kupata mikopo kwa wakati na kufanya shughuli zao kwa ubora na thamani.