MAFUNZO YA URASIMISHAJI WA BIASHARA NA UJUZI
- 18 December, 2025
Disemba 15, 2025, Afisa Mtendaji wa Mfuko wa Utamaduni, Bi. Nyakao Mahemba, lifungua Mafunzo ya Urasimishaji wa Biashara na Ujuzi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, yakilenga kutoa ujuzi wa ususi na ushonaji wa vikapu vya kisasa kwa wajasiriamali 40 kutoka Dar es Salaam na nje ya mkoa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Bi. Mahemba alisisitiza umuhimu wa urasimishaji wa biashara ndogondogo na za kati, akibainisha kuwa hatua hiyo husaidia wajasiriamali kupata fursa mbalimbali ikiwemo masoko rasmi, mikopo, na ushiriki katika maonesho ya kitaifa na kimataifa.
Mafunzo ya ususi wa vikapu ni sehemu ya programu ya Mafunzo ya Urasimishaji wa Biashara na Ujuzi yenye lengo la kuwajengea uwezo wajasiriamali katika kuendeleza na kurasimisha shughuli zao za kiuchumi. Kupitia mafunzo hayo, washiriki wanapata maarifa ya vitendo kuhusu mbinu bora za utengenezaji wa vikapu, ubunifu wa bidhaa, pamoja na masuala ya ujasiriamali na masoko.